Vitendawili 8 kwa Magufuli Zanzibar Imetolewa 28/12/2015
Rais Dk. John Magufuli
Wakati Rais Dk. John Magufuli, akikutana kwa nyakati tofauti na waliokuwa wagombea urais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Maalim Seif Sharif Hamad, wa Chama cha Wananchi (CUF), imefahamika kuwa Rais huyo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anakabiliwa na vitendawili takriban nane kuhusiana na hatma ya kisiasa kwenye visiwa hivyo.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwa kuhusisha mahojiano na wachambuzi kadhaa wa masuala ya siasa nchini umebainisha kuwa baadhi ya vitendawili hivyo vinavyotokana na mustakabali wa Zanzibar baada ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa visiwa hivyo uliofanyika Oktoba 25, 2015 ni pamoja na kujua ni vitu gani ambavyo Dk. Shein (CCM) na Maalim Seif (CUF) watakubali kuvipata au kuvipoteza baada ya kupatikana kwa suluhu ya mgogoro uliopo sasa. Uchaguzi ulifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, aliyeitaja sababu kuwa ni kwamba “haukuwa huru na wa haki”
Kadhalika, vitendawili vingine kwa Rais Magufuli ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu ni pamoja na kujua itakuwaje ikiwa Maalim Seif na Shein watashikilia misimamo yao, kwa maana kwamba, ikiwa Shein na wenzake CCM watasisitiza uchaguzi urudiwe huku Maalim Seif akikataa na kusisitiza kuwa mshindi wa Oktoba 25 atangazwe, nini kitakachofuata? Na je, ikiwa uchaguzi utarudiwa, msimamizi atabaki Jecha na makamishna wa ZEC walewale waliosababisha mgogoro uliopo sasa visiwani humo?
Aidha, katika uchunguzi wake huo, Nipashe imebaini vilevile kuwapo kwa kitendawili kizito kwa Rais Magufuli na serikali yake kuhusiana na namna ya kufanya sasa ili Zanzibari ibaki kuwa moja; Ni lini maridhiano yatafikiwa ili taifa lisikose ufadhili wa mashirika ya kimataifa kama MCC? Je, nini kifanyike ili doa la uchaguzi Zanzibar lisiendelee kuipunguzia Tanzania hadhi yake kuhusiana na demokrasia katika Jumuiya ya Kimataifa? Je, ikiwa mazungumzo yanayoendelea yatafikia makubaliano ya kurudiwa kwa uchaguzi, utafanyika lini ili kukidhi matakwa ya katiba?
Jumatatu iliyopita, Rais Magufuli alikutana na Maalim Seif katika Ikulu yake jijini Dar es Salaam na kuzungumza naye kwa dakika 135 kuhusiana na hali ya Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015’.
Kadhalika, kama ilivyokuwa kwa Maalim Seif, Rais Magufuli alikutana pia na Dk. Shein kwenye Ikulu yake jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya saa moja.
Mazungumzo ya Magufuli na wagombea hao yalihusina na hali ya visiwa hivyo baada ya kufutwa kwa uchaguzi, hususan mazungumzo yanayoendelea kwa nia ya kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinaendelea kudumishwa.
Akizungumza na Nipashe jana, Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu, Ombeni Sefue, alisema hatua ya Rais Magufuli kukutana kwa nyakati tofauti na Maalim Seif na Dk. Shein haimaanishi kwamba amechukua jukumu maalumu la kutafuta muafaka wa mgogoro wa kisiasa visiwani humo bali kupata maendeleo ya mazungumzo yanayoendelea kufanywa, chini ya usimamizi wa kamati maalum ya watu saba inayowahusisha pia marais wastaafu.
Balozi Sefue alisema Kamati Maalum iliyoundwa kushughulikia mgogoro huo inaendelea na kazi yake na mwelekeo wake ni mzuri katika kupata muafaka.
“Hadi sasa kamati maalum inaendelea vizuri na kazi yake. Walikuja kumhabarisha kinachoendelea, hawakuja kumkabidhi jukumu lolote maalum… nijuavyo kamati maalum inaendelea na kazi yake na mwelekeo ni mzuri,” alieleza Balozi Sefue, akikumbushia vikao nane vilivyofanywa hadi sasa na kamati hiyo maalumu kuanzia Novemba 9, 2015, ikiwahusisha Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi; Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete; Rais mstaafu wa Awamu ya Sita wa Zanzibar Dk. Amaan Abeid Karume, Rais mstaafu wa awamu ya tano wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour; Rais wa Zanzibar , Dk. Ali Mohamed Shein; Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na pia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.
Mgogoro wa Kisiasa uliopo sasa visiwani Zanzibar uliibuka mara baada ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi na Jecha. Mvutano uliopo sasa visiwani humo unatokana na msimamo wa Maalim Seif na chama chake (CUF) kusisitiza kuwa uchaguzi huo haukuwa na kasoro kubwa kiasi cha kufutwa wote na hivyo wanasisitiza kuwa ZEC iendelee na mchakato wa kukamilisha majumuisho ya kura na kumtangaza mshindi.
Hata hivyo, CCM wanapinga hoja ya CUF na kusisitiza kuwa uamuzi wa ZEC uheshimiwe kwa kufuta matokeo ya uchaguzi wa visiwa hivyo na kujiandaa kwa uchaguzi wa marudio.
Msimamo wa Maalim Seif na CUF yake umekuwa ukiongezwa nguvu na ripoti ya waangalizi wote wa uchaguzi huo kutoka ndani na nje ya ya nchi kusisitiza kuwa ulikuwa huru na wa haki na pia kushangazwa na uamuzi wa Jecha wa kufuta uchaguzi alioutoa Oktoba 28, 2015. Baadhi ya waangalizi hao walikuwa ni wa kutoka Jumuiya ya Ulaya (EU), Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na pia waangalizi wa ndani wakiwamo TEMCO.
VITENDAWILI KWA MAGUFULI
Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivu cha Sheria kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM0, Profesa Criss Maina, alisema kadri aonavyo, hakuna haja ya kurudia uchaguzi wote bali Serikali ya Rais Magufuli inapaswa kuongeza msukumo kuhakikisha kuwa mchakato unaendelea kuanzia pale ulipoishia.
Alisema katika majimbo ambayo yalishafanya uchaguzi, kazi ya kuhesabu kura iendelee kwa kuwa takwimu za wananchi wote zipo katika kampyuta.
Alisema Rais Magufuli anapaswa kuhakikisha kuwa anasaidia kulinda katiba ya Zanzibar badala ya kuwekwa kando kama alivyofanya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha.
Mbali na Prof. Maina, wachambuzi wengine wa masuala ya siasa waliotoa a maoni yao walipongeza mazungumzo yanayoendelea kwa nia ya kupata muafaka, huku wengine wakiainisha vitendawili ambavyo Rais Magufuli na serikali yake wanapaswa kuvitegua katika kipindi hiki cha kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.
NANI APATE NINI, APOTEZE NINI?
Swali mojawapo kubwa ni kwamba je, ni mambo gani Dk. Shein na Maalim Seif watayaridhia ili kufikia muafaka? Na je, hilo likitokea, ni nani atakubali apate nini na apoteze nini?
Wachambuzi wa masuala ya siasa za Tanzania, hasa visiwani, waliiambia Nipashe kuwa hiki siyo kitendawili chepesi na kwamba, kinahitaji subira na uvumilivu katika kutafuta muafaka.
Inaelezwa kuwa ugumu wa eneo hilo unatokana na ukweli kuwa wananchi wa Zanzibar ni wafuatiliaji wazuri wa masuala ya siasa na mara zote huwa na misimamo mikali linapokuja suala la itikadi za vyama vyao vikuu, yaani CCM na CUF.
“Mtihani ni kwamba, yeyote kati ya Shein na Seif watakuwa na kibarua cha ziada kujieleza kwa wanachama wao na kukubaliwa kuhusiana na maridhiano yoyote yanayogusa maslahi mapana ya CUF na CCM. Serikali ya Magufuli ina kazi kubwa ya kusaidia kupatikana muafaka katika eneo hilo ili kuleta utulivu Zanzibar,” mmoja wa wachambuzi alisema.
JE, ITAKUWAJE IKIWA MAALIM SEIF NA SHEIN WATASHIKILIA MISIMAMO YAO?
Inaelezwa kuwa hiki ni kitendawili kingine kigumu kinachohitaji kupatiwa majibu kungali mapema. Hadi sasa, mgogoro uliopo unatokana na Dk. Shein na kambi yake kusisitiza kuwa uchaguzi urudiwe kama ilivyoamuliwa na Mwenyekiti wa ZEC huku Maalim Seif na wenzake CUF wakisisitiza kuwa hakuna sababu ya kurudia uchaguzi bali mshindi atangazwe. Hoja ni kwamba je, ikiwa pande hizo mbili zitashikilia misimamo yao, ni nini kitafuata kuhakikisha kuwa umoja na mshikamano visiwani humo vinaendelea kudumishwa?
IKIWA UCHAGUZI URUDIWE, UTAFANYIKA LINI KUKIDHI MATAKWA YA KATIBA?
Novemba 12, mwaka huu, ZEC ilitangaza rasmi na kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi katika Gazeti la Serikali la Novemba 6, mwaka huu, na kueleza kuwa uchaguzi huo utarudiwa tena ndani ya siku 90.
Hadi kufikia leo, ni siku 82 zimepita tangu siku hiyo ya kutolewa tangazo katika gaeti la serikali, hivyo kubaki siku nane tu ili kukidhi matakwa ya katiba ya Zanzibar.
JE, NINI KIFANYIKE ILI DOA LA UCHAGUZI ZANZIBAR LISIICHAFUE NCHI KIMATAIFA?
Tangu aingie madarakani, Novemba 5, Rais Magufuli amejijengea sifa maeneo mengi Afrika na nje ya Affrika kutokana na staili yake ya kuchapa kazi, huku jitihada akizielekeza katika kuwanufaisha wananchi wa kawaida. Amekuwa katika nchi kama Afrika Kusini, Ghana, Australia, Kenya, Uingereza, Zimbabwe na hadi katika badhi ya vyombo vya habari nchini China. Hata hivyo, heshima ya nchi iko hatarini katika medani za kimataifa kutokana na tukio la kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kwa namna iliyoibua maswali mengi kwa wanaoheshimu misingi ya demokrasia.
JE, IKIWA UCHAGUZI UTARUDIWA, MSIMAMIZI ATABAKI JECHA NA ZEC HII AU?
Hiki ni kitendawili kigumu. Hii ni kutokana na ukweli kuwa mgogoro wa uchaguzi uliopo Zanzibar umesababishwa na tangazo la Jecha la kufuta uchaguzi huo Oktoba 28 kutokana na sababu mbalimbali alizotaja ikiwamo tuhuma kwa baadhi ya makamishna wa ZEC aliodai waliacha kufanya kazi yao kwa weledi na kutanguliza itikadi za vyama kiasi cha kukaribia kukunjana. CUF wameonyesha hawana imani na Jecha kutokana na tangazo lake la kufuta uchaguzi walioamini kuwa mgombea wao, Maalim Seif alikuwa ameshinda kwa zaidi ya asilimia 50.
Katika mazingira kama hayo, swali linaibuka kwamba je, ikiamuliwa uchaguzi urudiwe, ni nani watasimamia na kuaminiwa na pande zote hasa baada ya mvutano uliopo sasa?
JE, NINI KIFANYIKE ILI KULINDA UMOJA WA ZANZIBARI?
Hiki ni kitendawili kingine kinachohitaji majibu ya uhakika. Inaelezwa kuwa kwa wastani, wananchi wa Zanzibar wamegawanyika katika makundi makuu yaliyo sawa kiitikadi, ambayo ni CCM na CUF. Kwa sababu hiyo, uamuzi wowote ni lazima uheshimu matakwa ya pande zote ili kulinda umoja na mshikamano uliopo na kwamba, kinyume chake ni kukaribisha mgawanyiko usio na manufaa kwa taifa.
NI LINI MARIDHIANO YATAFIKIWA ILI TAIFA LISIKOSE UFADHILI KAMA WA MCC?
Athari zitokanazo na mgogoro wa kisiasa Zanzibar tayari zimeshaanza kujitokeza nchini baada ya Desemba 16, 2015, Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia la Serikali ya Marekani (MCC) kutoidhinisha msaada wa dola za Marekani 700 (takriban Sh. trilioni 1.5) kutokana na mgogoro huo. Fedha za msaada huo ni muhimu kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwamo ya usambazaji wa umeme vijijini. Kwa sababu hiyo, Rais Magufuli na serikali yake ana kitendawili cha kuhakikisha kuwa anasaidia kupatikana muafaka wa haraka Zanzibar ili taifa lisiathiriwe kwa kukosa misaada muhimu kama wa MCC.
USHIRIKI WA VYAMA VINGINE VYA SIASA
Wakati CCM na CUF wakiendelea na majadiliano yao kutafuta muafaka, swali jingine ni kwamba je, ni kwa namna gani maridhino watakayofikia yatahusisha pia vyama vingine vilivyosimamisha wagombea wao vikiwamo vya ADC na Tadea?
Comments
Post a Comment