MADHAIFU MATANO (5) YANAYODIDIMIZA MAHUSIANO NA NDOA
Makala hii ni tafakari huru kuhusu mambo ya msingi katika mahusiano. Hapa utapata tafakari ya maana ya maneno na imani ambazo zinatutatiza wengi wetu. 1. Mchanganyiko mkubwa kuhusu maana ya mahusiano, mapenzi na ndoa: Labda kipengele hiki tuanze kwa kueleza kuwa kunaweza kuwepo ndoa, lakini yasiwepo mahusiano wala mapenzi. Inaweza kuonekana kama inachanganya kidogo, lakini ndio ukweli wenyewe. Ndoa ni namna tuu ambayo wawili walio kwenye mahusiano wanaamua kuwataarifu rasmi watu wengine kuwa wao wapo rasmi katika mahusiano. Ndoa ni kiapo mbele ya watu wengine , na ni namna ya kutaka kumuhakikishia mwenza wako kuwa endapo kiapo hicho kitatokea kuvunjika, basi unakubali rasmi kuwajibika kwa mujibu wa taratibu zilizopo za ndoa husika, ikiwemo kukubali kuitwa kwenye mabaraza ya usuluhishi, kugawana mali, n.k. Na kwa upande wa kiroho, inabeba maana zaidi kuwa unaweka kiapo kwa Mungu wako kuwa utalinda mahusiano yako na huyo unayemchagua. Hivyo basi, ndoa haijengi ma...