Fahamu Jinsi ya kusisimua mapenzi msimu huu wa Krismasi

Jinsi ya kusisimua mapenzi msimu huu wa Krismasi




Wachumba
Wachumba wakifurahi pamoja wakiwa kitandani.

Kwa Mukhtasari

Msimu wa Krismasi umefika tena ambapo wapenzi hupumzika pamoja baada ya mwaka mzima wa pilkapilka za maisha.
https://www.facebook.com/nyota5blogspot https://twitter.com/Nyotafive

MSIMU wa Krismasi umefika tena ambapo wapenzi hupumzika pamoja baada ya mwaka mzima wa pilkapilka za maisha.
Ni msimu ambao wapenzi wanaweza kutumia kunogesha mapenzi ambayo wakati mwingine huingia doa kwa sababu tofauti.
Wataalamu wa mapenzi wanasema kuna njia nyingi za kukoleza mapenzi msimu huu.
Hata hivyo, wanaonya kwamba baadhi ya watu huishia kuvuruga uhusiano wa mapenzi badala ya kutumia msimu huu kuurutubisha.
Kwenye kitabu chake kuhusu uhusiano wa kimapenzi Dating in the High Season, mwandishi Peter Owen, aliye mtaalamu wa masuala ya mahaba aeleza kuwa watu wanaotumia msimu wa sherehe kuwaposa wachumba wao huwa na fursa nzuri ya kufurahia maisha ya ndoa.
Owen asema hii ni kwa sababu wakati wa sherehe hizi nyoyo za watu wengi huwa na furaha na kukubali kuwaposa wapenzi wao hutokana na hisia kali za ndani za mapenzi.
Hata hivyo, Owen anaonya wapenzi wapya dhidi ya kuposana msimu huu akisema msisimko wa sherehe huwazuzua wengi na kudhani wanaelea katika mapenzi ya dhati.
Akikubaliana na Owen, mtaalamu wa kituo cha Bighearts, Nairobi, Jessy Waka,  anasema watu wengi hujuta kwa kuwaposa vidosho katika hekaheka za sherehe za Krismasi.
“Baadaye wanagundua kuwa hakukuwa na mapenzi kati yao bali ulikuwa tu msisimko msimu huu washerehe na hawawezi kuvumiliana,” asema.

Zawadi
Kulingana na Bi Waka, japo zawadi ni muhimu katika kuimarisha uhusiano wa mapenzi, haitoshi msimu huu wa Krismasi wanavyodhani wanaume wengi.
“Kuna wanaume wanaodhani kumpa mpenzi zawadi Krismasi kunatosha.
Wanatoka kwenda kujivinjari na marafiki na kuacha wapenzi wao wakisononeka kwa upweke. Hili ni tendo hatari kwa huba,” asema.
Mtaalamu huyo asema watu wengi hutumia msimu huu kushiriki burudani maeneo ya mbali na nyumbani, wengine huwa wanahudhuria ibada ya kushukuru Mungu na wengine huandaa vikao vya pamoja vya familia.
“Hizi ni baadhi ya mbinu za kuwasha moto wa mapenzi. Kwa kuwa watu wengi huwa katika likizo ndefu, huu ni msimu mzuri wa kuwasha upya moto wa mapenzi.
“Ingawa wengi huamua kwenda kujivinjari maeneo ya burudani mbali na nyumbani, kula na kucheza pamoja, lengo linapasa kuwa kunogesha mapenzi ambayo huzimika kutokana na shughuli za mwaka,” asema Bi Waka.
Anasema wachumba wakitumia vyema msimu wa Krismasi wanaweza kuamsha msisimko wa mahaba.
“Unaweza kufanya hivi kwa mambo mengi kama kumnunulia mpenzi wako zawadi atakayokumbuka kwa muda mrefu na ndivyo watu wengi hufanya,” asema.
Bi Waka anasema ni muhimu watu kuhakikisha hawavurugi hisia za mapenzi za wachumba wao kwa kukosa kuwashirikisha katika maandalizi ya mipango ya Krismasi.

Ratiba
“Zawadi pekee haitoshi kumridhisha mpenzi msimu wa sherehe ambao kilele huwa ni Desemba 25.
Kuna haja ya kupanga ratiba yenu pamoja na kwa muda unaofaa,” asema na kuongeza kuwa watu wengi hasa wanaume huwashurutisha wanawake kufuata waliyopanga.
“Kilicho muhimu ni kujadiliana kwa kina kabla ya kupanga ratiba ya sherehe.
Inafaa mtu kusaka maoni ya mpenzi wake hata kabla ya kumnunulia zawadi,” asema Bi Waka.
Kwa kufanya hivi, aeleza, ni muhimu kuzingatia maoni ya kila mmoja wenu.
Wengi huvuruga msimu wa sherehe kwa kushinikiza wapenzi wao kukubali maoni yao.
Kulingana na Emmy Njenga, mtaalamu wa kituo cha Maisha Mema, kumshinikiza mwenzio kukubali maoni yako ni kumkosesha furaha msimu huu wa sherehe na kuhatarisha penzi.
Anasema watu wengi hukosea kwa kuwaalika wageni tele nyumbani na kusahau kwamba wapenzi wao wanawahitaji msimu huu wa sherehe.
“Hakuna ubaya kujumuika na watu wa familia au marafiki wa dhati nyumbani kwa sherehe za Krismasi lakini ipo haja ya wachumba kutenga  muda wao wenyewe.
“Kuna watu wanaowapatia kipaumbele marafiki na wazazi wao kuliko wapenzi wao msimu wa sherehe za Krismasi. Hili ni kosa kubwa ambalo ni rahisi kuyeyusha upendo,” aeleza Bi Njenga.
Anasema vikao vya familia ni sehemu ya kusherehekea msimu huu hasa katika jamii za kiafrika.
Kulingana na Bi Njenga msimu wa sherehe za mwisho wa mwaka huwa ni wakati mzuri kwa wanaonuia kuoana kudhihirisha penzi lao.
Wengi hutumia msimu huu kuwatambulisha wapenzi wao kwa wazazi au jamaa zao.
Kujuana zaidi
“Wanaweza  kutumia msimu huu kujuana zaidi. Ikiwa wanapanga kuona wanaweza kuwatambulisha wachumba wao kwa wazazi na kukoleza huba,” asema Bi Njenga.
Kulingana na wataalamu wa mapenzi adui mkubwa wa mapenzi msimu wa Krismasi ni upweke.
“Usimhepe mchumba wako msimu wa sherehe. Kumwacha mpenzi katika lindi la upweke msimu huu ni kusambaratisha penzi,” asema Bi Waka kauli ambayo David Kirui anaiunga mkono.
 “Ni rahisi mpweke kuamini hapendwi. Hivyo basi ni muhimu kuwa na mipango thabiti ya kumtumbuiza mpenzi wako na kutia makali penzi lenu,” asema.
Bw Kirui anasema watu wengi huamua kuwahepa wapenzi wao wakikosa pesa za kwenda kujivinjari. “ Badala ya kumhepa, mweleze ukweli wa mambo na kama naye anakupenda, atakuelewa,” asema Bw Kirui.
Anasema mtizamo ya watu kuhusu maisha ni tofauti na kila mmoja anafaa kutambua na kuheshimu hulka za mpenzi wake.
“Kuna wanaofurahia kushehenezewa zawadi za kifahari na wengine hawapendi. Kuna wanaopenda kwenda maeneo ya burudani na wengine makanisani na kuna wanaopenda kubarizi nyumbani,” asema.

Comments

Popular posts from this blog

TAZAMA PICHA 30 ZA MREMBO AGNES MASOGANGE AKIJIACHIA KISTAA NJE YA NCHI

Gamboshi: Makao Makuu ya Uchawi na Wachawi yaliyopo Shinyanga, Tanzania

14 parties want Parliament to discuss Zanzibar impasse