Kujiuzulu kwa Waiguru kulivyopisha mabadiliko

Bi Anne Waiguru
Waziri wa Ugatuzi Bi Anne Waiguru muda mfupi kabla ya kujiuzulu Novemba 21, 2015. Picha/WILLIAM OERI 
Na CHARLES WASONGA
Imepakiwa - Sunday, November 29  2015 at  14:53
Kwa Mukhtasari
Kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi  Bi Anne Waiguru ndiko kuliwachochea Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kuafikiana haraka kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri Jumanne baada ya shughuli kucheleweshwa kwa miaka kadhaa, wabunge na wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema.

KUJIUZULU kwa aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi  Bi Anne Waiguru ndiko kuliwachochea Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kuafikiana haraka kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri Jumanne baada ya shughuli kucheleweshwa kwa miaka kadhaa, wabunge na wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema.
Kuondoka kwa waziri huyo kuliacha baraza hilo na mawaziri 13  pekee ikizingatiwa kuwa mawaziri 5 walisimamishwa kazi mapema mwaka huu kwa tuhuma za ufisadi.
Na kwa mujibu wa wakili Bobby Mkangi, baraza hilo halikuwa kamilifu kikatiba kwani idadi hiyo haipasi kupungua 14 au kuzidi 22.
Muungano wa Cord nao ulianza kuisuta Serikali kuhusiana na upungufu huo huku wakimtaka Rais Kenyatta kubuni baraza jipya la mawaziri lisilo na watu wenye madoadoa ya ufisadi.
Duru ziliambia Taifa Jumapili kwamba, kabla ya kujiondoa kwa Waiguru, wawili hao wamekuwa wakitofautiana, japo kichinichini, kuhusu hatima ya watano hao, teuzi katika nyadhifa zingine za umma na wazo la kugawanywa kwa Wizara ya Ugatuzi, iliyokuwa chini ya Bi Waiguru.
Hata hivyo, Ikulu ya Rais ilipinga madai hayo ikisema serikali ni thabiti na mabadiliko yatafanyika “kwa hiari ya Rais.”
Tangu Julai, Rais amekuwa akitarajiwa kufanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri baada ya makataa ya siku 60 aliyotoa kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kukamilisha uchunguzi kuhusu kesi za ufisadi dhidi ya maafisa 175 wa serikali waliotajwa kwenye ripoti aliyowasilisha bungeni Machi 26, 2015.
Miongoni mwao walikuwa mawaziri watano; Michael Kamau (Uchukuzi), Charity Ngilu (Ardhi), Kazungu Kambi (Leba), Felix Koskei (Kilimo) na Davis Chirchir (Kawi).
Majuzi, watano hao walitemwa Rais alipotangaza baraza jipya la mawaziri ambapo watu saba wapya waliteuliwa huku wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia ikibuniwa.
Wageni hao ni; Dan Kazungu (Uchimbaji Madini), Willy Bett (Kilimo), Mwangi Kiunjuri (Ugatuzi na Mipango), Charles Keter (Kawi na Mafuta),  Dkt Cleopas Mailu (Afya)  Bi Sicily Kariuki (Utumishi wa Umma) na Joe Mucheru (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano).
Uvumi kuhusu mabadiliko hayo ulishika kasi baada ya Mbw Koskei na Chirchir na Kambi kuondolewa lawamani, kuripotiwa kwa sakata ya kupotea kwa Sh971 milioni katika Shirika la Vijana kwa Huduma ya Kitaifa (NYS) na wabunge wa URP kutoka Rift Valley kuanza kushinikiza kurejeshwa kazini kwa Koskei na Chirchir.
“Ndio, tulitaka Mbw Koskei na Chirchir warejeshwe kazini kwa kuwa EACC na Afisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) Keriako Tobiko ziliwaondolewa lawama kuhusu madai ya ufisadi yaliyowakabili.
Na kwa upande mwingine binafsi, niliwasilisha hoja bungeni nikitaka Bi Waiguru asimamishwe kazi ili achunguzwe kuhusu sakata kadha katika wizara aliyosimamia, ikiwemo ile ya kupotea kwa Sh791 milioni,” alisema Mbunge wa Nandi Hills Alfred Keter.
Japo Chirchir aliondolewa makosa ya kujaribu kudai kiinua mgongo cha Sh1.4 bilioni kutoka na zabuni ya Sh52 bilioni iliyotolewa na kampuni ya kusafirisha mafuta kupitia mabomba, Kenya Pipeline, bado anachunguzwa kuhusiana na kashfa ya kupokea hongo alipokuwa kamishna wa iliyokuwa Tume ya Muda ya Uchaguzi na Mipaka (IIBC), almaarufu “Chickengate”.
Alizuia mabadiliko
Wabunge kutoka Rift Valley walisema kujiuzulu kwa Bi Waiguru kulipokelewa na furaha katika maeneo yao kwa sababu, alivyosema mmoja wao, “sababu huyo mama ndiye alizuia mabadiliko katika baraza la mawaziri kwa sababu alikataa kukaa kando kama mawaziri wengine licha ya wizara yake kuzongwa na ufisadi.”
“Rais alionekana wazi kumkinga hali ambayo ilitufanya kuamini kuwa vita dhidi ya ufisadi ilikuwa ikiendeshwa kwa njia ya mapendeleo.
Kimsingi, Koskei na Chirchir wangerejeshwa kazini kwa sababu walikuwa wasafi baada ya kuondolewa tuhuma za ufisadi,” akasema mbunge huyo wa ambaye aliomba tulibane jina lake.
Ilisemekana Bw Ruto pia alitaka wawili hao, ambao ni washirika wake wa karibu, warejeshwe kazini lakini Rais Kenyatta na washauri wake walisemekana kukataa pendekezo hilo. 
Rais alihisi kuwa kurejeshwa kwa mawaziri hao kungetoa ujumbe mbaya katika vita dhidi ya ufisadi ikizingatiwa kuwa tayari serikali ilikuwa ikishutumiwa na upinzani pamoja na mabalozi wa kigeni kwa “kumlinda Waiguru”.
Kulingana na mchanganuzi Profesa Edward Kisiang’ani, hali hii ndio ilisababisha naibu rais kuamua kuweka “presha” kwa mkubwa wake kupitia wabunge kutoka ngome yake ya Rift Valley.
Na mwezi Oktoba wabunge, Elisha Busienei (Turbo), Silas Tiren (Moiben), Cornel Serem (Aldai), Ronald Tonui (Bomet ya Kati) na Seneta wa Nandi Stephen Sang’ walidai Koskei alipasa kurejeshwa afisini ili akabiliane na changamoto katika sekta ya kilimo.
“Ukweli ni kwamba ilifika wakati Naibu Rais alilazimika kuwasiliana na mkubwa wake kupitia wabunge kutoka sehemu anakotoka.
Japo alimpigia debe Bi Waiguru, hali ilikuwa vingine nyuma ya pazia,” anasema msomi huyo.
Vuta nikuvute
Mhadhiri huyo anakubali kuwa vuta nikuvute hiyo ndio iliyokuwa ikitibua mipango ya rais kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri kwa mara kadha tangu mapema Septemba.
Kwa mfano, mnamo Septemba 20, Rais alitaka kutangaza mabadiliko serikalini kwa kuwapiga kalamu mawaziri wote 5 waliosimamishwa kazi Machi 26, lakini ilisemekana kuwa Bw Ruto alidinda kwenda Ikulu kwa shughuli hiyo.
Kamera za runinga ya KBC zilikuwa zimewekwa Ikulu kufikia saa mbili asubuhi tayari kwa shughuli hiyo lakini Ruto hakuonekana.
Rais Kenyatta alipokuwa akisubiri kufika kwake Ikulu ya Nairobi kwa zoezi hilo, Bw Ruto alikuwa katika makao yake rasmi mtaani Karen, akikutana na viongozi wa kisiasa na wataalamu kutoka  Rift Valley. Duru zilisema Rais alitaka kukamilisha kibarua hicho kabla ya kwenda jijini New York,  Amerika kwa Kongamano la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Kinaya ni kwamba, saa mbili usiku siku hiyo Ruto alikuwepo wakati Rais akihutubia taifa kuhusu mgomo wa walimu na kabla.
Mkinzano wa kimawazo katika ya Rais na Naibu wake wakati huo ulitajwa kama tisho kwa uthabiti wakati huo ambapo serikali ilikuwa inakabiliwa na changamoto ya mgomo wa walimu na njama ya upinzani ya kupitisha kura ya kutokuwa na imani kwa Rais Kenyatta.
Hii ni kando na shinikizo za Alfred Keter dhidi ya Bi Waiguru.
Kulingana na Kisiang’ani, baada ya Waiguru kujiuzulu kutokana na kile alichodai kuwa ushauri kutoka daktari wake, Rais na Naibu wake hawakuwa na budi ile “kuelewana” kuhusu mabadiliko katika baraza la mawaziri.
“Iliwabidi kuelewana haraka iwekekanavyo kwa sababu baraza la mawaziri lilibaki gofu, likiwa na mawaziri 13 pekee kinyume cha Katiba. Ilikuwa ni hali ya nipe nikupe.
Naibu Rais alikubali kuachilia Koskei, Chirchir na Kambi huku Rais akikubali wizara ya ugatuzi igawanywe mara mbili,” akasema.
Hii ndio sababu mpya ya Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia iliyobuniwa na ikapewa Bi Kariuki ambaye alikuwa Katibu katika wizara ya Kilimo. Idara ya NYS ilizongwa na kashfa za ufisadi iko chini ya wizara hii mpya.
Joseph Chumba, mtaalamu katika masuala ya uongozi, anasema Bw Ruto aliamua kumteu mwandani wake, Charles Keter, ili azime joto la kisiasa ambalo limekuwa lichochewa na Gavana wa Bomet katika eneo la South Rift.
Barua Pepe: cwasonga@ke.nationmedia.com

Comments

Popular posts from this blog

TAZAMA PICHA 30 ZA MREMBO AGNES MASOGANGE AKIJIACHIA KISTAA NJE YA NCHI

Gamboshi: Makao Makuu ya Uchawi na Wachawi yaliyopo Shinyanga, Tanzania

14 parties want Parliament to discuss Zanzibar impasse