Drogba sasa alenga kuchukua mikoba ya Mourinho
Mshambuliaji wa Ivory Coast Didier Drogba akichapa mpira mbele ya rais wa klabu ya Montreal Joey Saputo (kushoto) Julai 29, 2015 mjini Montreal. Picha/AFP
Kwa Mukhtasari
Mshambuliaji Didier Drogba analenga wadhifa wa Kocha Mkuu katika klabu yake za zamani Chelsea.
MSHAMBULIAJI Didier Drogba analenga wadhifa wa Kocha Mkuu katika klabu yake za zamani Chelsea.
Drogba, ambaye wakati huu anacheza kandanda ya malipo nchini Canada, anasema ameafikiana na waajiri wake wa zamani kurudi Stamford Bridge kama kocha atakapotundika daluga zake.
Raia huyu wa Ivory Coast alipachika mabao 164 alipokuwa Chelsea. Katika mahojiano na shirika la BBC, mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 37 alisema, “Nataka kusaidia klabu ambayo imenijenga sana. Nimekubaliana na wakurugenzi wa Chelsea.”
“Mbona nisiwe kocha? Mbona siyo mkurugenzi, mkufunzi katika shule ya kunoa chipukizi au hata kutwikwa majukumu ya kushauri washambuliaji?”
Drogba alifunga penalti iliyosaidia Chelsea kunyanyua kombe la Klabu Bingwa Ulaya mwaka 2012 na pia akashinda taji lake la nne la Ligi Kuu ya Uingereza baada ya kurudi Stamford Bridge msimu uliopita kabla ya kujiunga na Montreal Impact katika Ligi Kuu ya Amerika na Canada almaarufu MLS.
Hata hivyo, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza, Chelsea, wamekuwa na msururu wa matokeo duni msimu 2015/16. Walipoteza mechi saba kati ya 12 zao za mwanzo na wanakamata nafasi ya 15 kwenye jedwali.
Drogba amekuwa akiunga mkono kocha Jose Mourinho, akisema yeye “bado ndiye kocha anayefaa” kuongoza Chelsea na kusisitiza anaamini wachezaji pia wanaunga mkono Mreno huyo licha ya uvumi kuwa kuna mgawanyiko mkubwa kikosini.
“Kama klabu bado imemkwamilia inamaanisha mmiliki Roman Abramovich anaamini kuwa yeye ndiye anayefaa kushikilia wadhifa huo,” alisema.
“Nadhani wachezaji wanamuamini na anajitolea kwa dhati kubadilisha hali ilivyo.” Drogba alikiri Chelsea inapitia “wakati mgumu” msimu huu, lakini kushinda mara mbili mfulilizo dhidi ya Norwich na Maccabi Tel Aviv ni ishara mambo yanabadilika.
“Wana wachezaji wazuri na pia maafisa wa kiufundi wenye ujuzi mwingi,” aliongeza. “Klabu hii si klabu ambayo inakuwa na masaibu mara mbili katika msimu mmoja.”
Comments
Post a Comment