Van Gaal aomba radhi kwa kujiangusha
Van Gaal aomba radhi kwa kujiangusha
MANCHESTER, ENGLAND
KOCHA wa Manchester United, Van Gaal, ameomba radhi kwa kitendo cha kujiangusha juzi mbele ya mwamuzi wa akiba, Mike Dean, katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Arsenal, kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Kocha huyo alijiangusha kwa makusudi huku akiwa na lengo la kumuonesha mwamuzi jinsi wachezaji wa Arsenal wanavyojiangusha kwa kumdanganya mwamuzi wa mchezo huo.
Kocha huyo alimwambia mwamuzi kwamba mshambuliaji wa Arsenal, Alexis Sanchez, amekuwa mjanja hivyo mara kwa mara anajiangusha kwa ajili ya kuomba ili waweze kutumia mipira ya adhabu.
Hata hivyo, Van Gaal amekiri kwamba alifanya makosa kuonesha mfano huo mbele ya mashabiki ambao walionekana kushangilia.
“Halikuwa jambo zuri kufanya mbele ya mwamuzi wa kati, mshika kibendera na mwamuzi wa akiba, ninakubali kwamba nilifanya makosa na natumia muda huu kuomba radhi kwa kitendo ambacho nilikifanya, japokuwa mashabiki walionekana kufurahia.
“Nilifanya vile kutokana na hisia kali ambazo nilikuwa nazo kwa wakati ule kutokana na mambo ambayo wachezaji wa Arsenal walikuwa wanayafanya, lakini baada ya muda nikagundua kuwa si jambo zuri,” alisema Van Gaal.
Comments
Post a Comment