Umesikia hii>>>>>Kigogo bomoabomoa arejeshwa kazini. Soma zaidi Hapa
Siku chache baada ya Ofisi ya Makamu wa Rais,
Muungano na Mazingira, kuwasimamisha kazi, vigogo watatu wa Baraza la
Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), Kigogo aliyekuwa akisimamia
bomoabomoa amerudishwa kazini, imebainika.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani zilizolifikia Nipashe zinaeleza
kuwa, kigogo aliyerudishwa kazini siku nne tu mara baada ya kusimashwa
kazi ni Mwanasheria Mkuu wa Nemc, Heche Suguta. Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira(Nemc)
Chanzo hicho kilieleza kuwa, Suguta alirudi kazini Januari 29, siku
nne baada ya wizara hiyo kutangaza kumsimamisha kazi ili kupisha
uchunguzi baada ya kutuhumiwa kukiuka miiko ya kazi katika kusimamia
kiwanda cha Kusindika Minofu ya Punda kilichopo mkoani Dodoma.
“Heche yuko kazini tangu Ijumaa ya wiki iliyopita, alikaa nyumbani
siku nne tu, ila hatufahamu nini kilitokea juu ya hilo,” kilibainisha.
Chanzo hicho kilieleza kuwa, hawana taarifa za maofisa wengine kama watarudishwa kazini au laa.
Mkurugenzi Mkuu wa Nemc, Bonventure Baya, alipoulizwa na Nipashe
kuhusu suala la ofisa huyo kurudishwa kazini, alisema hawezi kuzungumzia
jambo hilo kwa madai kuwa liko juu ya uwezo wake.
“Jambo hilo siwezi kulizungumza liko juu ya mabosi wangu, hivyo siwezi kusema chochote juu ya hilo,” alisema Baya.
Nipashe pia lilimtafuta Suguta ili kuzungumzia suala hilo, lakini simu yake iliita bila majibu na baadaye ilizimwa.
Maofisa wa wizara hiyo nao walitafutwa ili kuzungumzia jambo hilo, bila ya mafanikio, hadi Nipashe linakwenda mitamboni.
Wengine waliokuwa wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi ni
Ofisa Mazingira Mwandamizi, Dk. Eladius Makene na Ofisa Mazingira,
Boniface Benedict Kyaruzi.
Katika adhabu hiyo, pia Baya, alitakiwa kuandikiwa barua ya onyo
kali la mwisho kwa tuhuma ya udhaifu wa usimamizi wa watumishi wa Nemc,
hivyo kusababisha malalamiko mengi kuhusu utendaji wa Baraza hilo.
Kuhusu kiwanda cha Kusindika Minofu, taarifa hiyo ilisema
imegundulika kuwapo kwa ukiukwaji mkubwa wa makusudi na wa wazi wa miiko
ya kazi kwa watumishi wa Nemc.
Aidha, wizara iliagiza kuwa ndani ya wiki moja Nemc ipitie upya
orodha ya wataalam na taasisi elekezi, zilizosajiliwa na kufuta wataalam
na taasisi zote ambazo zimekuwa zikikiuka maadili ya kazi zao.
Comments
Post a Comment