Chadema yamtaka Lubuva kuwa mkweli SoMA Zaidi Hapa>>>
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Damian Lubuva.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemtaka Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Damian Lubuva, kuwa mkweli na
kuacha kuudanganya umma juu ya kuingiliwa kwa tume wakati wa Uchaguzi
Mkuu.
Taarifa ya chama hicho kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana
jijini Dar es Salaam na Meneja Mawasiliano, Tumaini Makene, imeeleza
kuwa kuingiliwa kwa tume siyo lazima kuwapo maelekezo maalum
yanayotolewa wazi na kwamba hata kunyimwa bajeti ambayo imepitishwa na
Bunge na kuchelewesha utekelezaji wa majukumu ikiwamo vifaa vya BVR ni
mojawapo ya dalili za wazi kuwa tume haiko huru.
Alibainisha sifa nyingine kuwa ni kubadilishwa kwa watendaji wa
tume katikati ya mchakato wa uchaguzi, kwani wengi walibadilishwa mwezi
mmoja kabla ya uchaguzi kinyume cha kanuni za maadili ya uchaguzi.
“Hadi leo Nec imeshindwa kutoa sababu zozote za maana kuhalalisha
uteuzi huo ambao uliwaondoa watumishi waliokuwapo na kuwekwa watu
waliodaiwa kutoka vyombo vya dola,” alisema.
Aidha, alisema jingine ni Jaji Lubuva alivyonukuliwa wakati akitoa
maoni yake kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kuwa alikiri tume haiko
huru na kutaja sababu kadhaa kama uteuzi wa wajumbe wa tume, uthibitisho
na namna wanavyoapishwa kwani wanalazimishwa kuwa watiifu kwa rais
aliyewateua na kuwaapisha wakati ni mwenyekiti wa chama cha siasa.
Kuhusu suala la Zanzibar, Makene alisema Jaji Lubuva amepotosha
kwani Watanzania wanapomtaka Rais Dk. John Magufuli, aingilie kati suala
la mgogoro wa kisiasa Zanzibar, hawasemi ielekeze Nec namna ya
kuendesha uchaguzi bali yako masuala ya msingi yanayomhusu moja kwa moja
yeye kama rais na Amiri Jeshi Mkuu.
Aliyataja baadhi ya masuala hayo kuwa ni matumizi ya vyombo vya
dola yanayoendelea visiwani humo kinyume cha sheria na utawala wa sheria
na demokrasia, tume kutoa tamko chini ya ulinzi, kuendelea kuzagaa kwa
askari wakitisha wananchi ni masuala ambayo hayawezi kutokea bila kuwspo
kwa amri.
“Pia uvunjifu mkubwa wa Katiba na Sheria katika kufutwa kwa
uchaguzi wa rais Zanzibar na kuitishwa upya, kunamweka mahali anatakiwa
kuonyesha kuwa anawajibika kuilinda Katiba ya nchi,” alisema.
Juzi, Jaji Lubuva alikutana na Rais na kueleza kuwa tume iko huru na haijawahi kuingiliwa.
Comments
Post a Comment