Mzee wa Vijisenti (CHENGE) Escrow yamlipukia bungeni. Soma Zaidi HAPA
Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.
Chenge alikutwa na masahibu hayo wakati wa kujieleza na baadaye
kuulizwa maswali alipokuwa akiomba kura kwa ajili ya kuchaguliwa kuwa
mwenyekiti wa bunge. Mwanasheria huyo mkongwe alipendekezwa na Kamati ya
Uongozi wa Bunge kuwania nafasi hiyo.
Baada ya kujieleza ili kushawishi wabunge wamchegue katika nafasi
hiyo, ulifika wakati wa maswali ambapo wapinzani walimuuliza kuhusu
kashfa ya Tegeta Escrow.
Hatua hiyo ilisaababisha kuchafuka kwa hali ya hewa ndani ya bunge
baada ya kuibuka zomeazomea kati ya wabunge wa CCM waliokuwa wakipinga
baadhi ya maswali ya wale wa upinzani walioonekana kumkamia Chenge.
Bunge lililopita baada ya kujadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu miamala iliyofanyika kwenye
Akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), lilipitisha maazimio manane likiwamo la kuwajibishwa viongozi wa
serikali na wale wa Kamati za Bunge walioonekana kuhusika katika kashfa
hiyo.
Viongozi wa kamati ambao Bunge liliazimia wawajibishwe ni pamoja na
Chenge, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti.
Wengine ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Katiba, Sheria na
Utawala, William Ngeleja, na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa.
Katika kashfa ya Escrow, Chenge alidaiwa kupokea Sh. bilioni 1.6
kutoka kwa james Rugemalira, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya VIP
Engineering and Marketing Limited, iliyokuwa na asilimia 30 kwenye
Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), inayodaiwa kuuzwa
kinyemela kwa Kampuni ya Pan African Power (PAP).
Jana, hali ya hewa bungeni ilianza kuchafuka pale Chenge
alipomaliza kujieleza kwa wabunge na Spika Job Ndugai kuruhusu aulizwe
maswali, hatua iliyofanya wabunge wengi wa upinzani kusimama kutaka
kupewa nafasi huku wale wa CCM wakiwa wameketi.
Mbunge wa kwanza aliyepata nafasi ya kuulizwa swali ni wa Ndanda
(CHADEMA), Cecil Mwambi, ambaye alimtaka Chenge kujibu suala la Escrow
likirudi bungeni, kama ataweza kulisimamia ilhali aliwajibishwa na Bunge
kwa sababu ya kashfa hiyo.
Akijibu swali hilo, Chenge alisema Bunge linaendeshwa kwa kanuni
ambazo baadhi yake zinasema kama kuna suala linajadiliwa na una masilahi
nalo, ni vyema ukakaa pembeni na kuacha lijadiliwe.
“Linapokuwa suala ambalo una maslahi nalo, ni bora ukakaa pembeni
ili uendeshwaji wa shughuli za Bunge usiwe na makandokando, ningeweza
kuendelea kuzungumza sana, lakini ngoja niishie hapa,” alisema Chenge.
Baada ya swali hilo, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Latifah
Chande, alikoleza moto kwenye hoja ya Escrow alipomwuliza Chenge kama
haoni kuwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge ilhali alikuwa kwenye
kashfa hiyo ambayo ilijadiliwa na wananchi walio wengi, kutashusha hadhi
ya chombo hicho cha kutunga sheria.
“Huoni kwamba wananchi watakosa imani na Bunge hili litakalokuwa likiongozwa na mtu kama wewe?” alihoji Latifah.
Swali hilo lilionekana kuwasha moto zaidi bungeni huku wale wa CCM wakianza kupiga kelele kwa kudai kwamba hilo si swali.
Spika Ndugai aliyekuwa akiongoza kikao hicho cha asubuhi, hakutoa
nafasi kwa Chenge kujibu swali hilo na badala yake akamruhusu Mbunge wa
Mtwara Vijijini (CCM), Hawa Ghasia, kuuliza swali lingine.
“Ratiba inaonyesha baadaye kutakuwa na mjadala wa kuchangia hotuba
ya rais na wakati alivyokuja kuhutubia hapa kuna watu walitoka nje ya
Bunge. Je, ukiwa mwenyekiti utawaruhusu kuchangia hotuba hiyo?” aliuliza
Hawa.
Swali hilo lilionekana kuwakera wabunge wa upinzani ambao walianza
kumzomea mbunge huyo huku wengine wakisema “ndiyo maana uliachwa (kwenye
uteuzi wa mawaziri),… umekosa sifa.”
Swali hilo lilijibiwa na Ndugai aliyesema kila mbunge atakuwa na haki ya kuchangia kwenye hotuba hiyo ya Rais.
Wengine waliopendekezwa na Kamati ya Uongozi kuwania nafasi hiyo ni, Mary Mwanjelwa na Najima Murtaza Giga.
Mbali na uenyekiti wa Bunge, Chenge pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo.
Kwa kuwa wenyeviti wa Bunge wanaotakiwa ni watatu na
waliopendekezwa kushika nafasi hiyo ni idadi hiyo hiyo, wabunge
hawakupiga kura na badala yake, baada ya kujieleza na kuulizwa maswali,
spika alihoji Bunge zima juu ya wanaokubali kuwa wabunge hao washike
nafasi hizo.
Wenyeviti wa Bunge pamoja na mambo mengine, huongoza vikao vya
Bunge pale spika na naibu wake wanapokuwa hawapo bungeni na
wakishachaguliwa hushika nafasi hiyo kwa miaka miwili na nusu.
Hali ya Zanzibar
Wabunge wa upinzani waliopata nafasi ya kuchangia hotuba ya Rais
John Magufuli, pamoja na mambo mengine, walizungumzia hali ya kisiasa
Zanzibar wakisema ni vyema ikashughulikiwa mapema.
Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea (CUF), alisema kitendo cha Rais
Magufuli kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge kusema suala la
Zanzibar linashughulikiwa na CCM na CUF, kinaonyesha kwamba anajitoa
kwenye mgogoro huo.
Alisema maelezo hayo ya Rais juu ya Zanzibar yaliyo ukurasa wa 10
wa hotuba yake, yanaaonyesha kwamba anataka kulikwepa suala hilo.
“Jambo kama hili utaliachaje kwa Serikali ya Zanzibar? Sehemu moja
ya Muungano ikiingiwa na machafuko kwingine hakutakuwa salama,”
alisema.
Naye Mbunge wa Mbozi (Chadema), Paschal Haonga, aliitaka serikali
kutangaza mapema mshindi pindi uchaguzi unapofanyika kwa kuwa mara
nyingi hali ya kuchelewesha matokeo huleta machafuko.
Alisema anashangaa Rais Magufuli kusema uchaguzi ulikuwa huru na
ulitawaliwa na amani wakati kuna sehemu watu wamekimbia makazi yao kwa
sababu ya uchaguzi na mpaka sasa hali ya Zanzibar haieleweki.
Mbunge mwingine aliyezungumzi hali ya Zanzibar ni Suleiman Sadick
wa Mvomero (CCM), ambaye alisema ni vyema Rais Magufuli akaachwa
aendelee na mambo mengine huku Wazanzibari wakijiandaa na uchaguzi wa
marudio.
“Uchaguzi wa Zanzibar ni wa kisheria na umefutwa kwa sababu ya
mizengwe iliyokuwapo. Tusubiri Machi 20 uchaguzi wa marudio ufanyike.
Sisi tuwaombee Wazanzibari uchaguzi mwema,” alisema.
Mbali na mambo mengine, Mbunge wa Temeke, Mtolea, alipokuwa
akichangia alisema Rais Magufuli badala ya kusema tu ataanzisha Mahakama
ya Mafisadi, ajikite kuhakikisha kesi za watuhumiwa wa wauaji wa albino
zinaendeshwa haraka na waliohukumiwa kunyongwa wanyongwe.
Alisema Rais ndiye mwenye mamlaka ya kuruhusu watu hao kunyongwa na hatia hiyo itasaidia kupunguza vitendo hivyo vya mauaji.
Comments
Post a Comment