John Magufuli » Kimbunga cha Magufuli chatua Mashirika ya Umma, ATCL, TRL And Tazara Matumbo Moto
Kimbunga cha Magufuli chatua Mashirika ya Umma, ATCL, TRL And Tazara Matumbo Moto
Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru amezitaka taasisi na mashirika ya umma nchini kuacha utegemezi kwa Serikali, badala yake kupunguza matumizi na wafanyakazi ili kuongeza mapato na ufanisi.Mafuru alisema Serikali imebeba mzigo wa taasisi na mashirika hayo kwa kutegemea izipatia fedha kutoka Hazina kwa ajili ya kujiendesha, na kulipa mishahara ya wafanyakazi na kusababisha ufanisi wao kuwa mdogo.
Mafuru pia alitangaza kufuta posho za wabunge katika bodi za mashirika na kuanzisha mchakato wa kuwaondoa katika mashirika hayo, ili wabaki na jukumu lao la msingi la kuikosoa Serikali badala ya kuingia katika utendaji.
Kuhusu uzalishaji
Msajili huyo alisema inashangaza kuona kwamba mpaka sasa kuna mashirika ya umma ambayo bado yanaitegemea Serikali kulipa mishahara ya wafanyakazi wake.
Aliyataja mashirika hayo kuwa ni Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Kampuni ya Hifadhi za Reli (RAHCO) na Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (Tazara).
Alisema hakuna haja kwa Serikali kuendelea kuwa na mizigo hiyo isiyozalisha ikiwamo kubeba gharama za kuendesha mashirika hayo.
“Wenyeviti na wajumbe wa bodi, pamoja na watendaji wakuu wa kila shirika mkae chini mjitafakari, kwa nini muendelee kuongoza mashirika hayo wakati mmeshindwa kuzalisha. Rais ameniagiza kuwakumbusha kwamba mrejee malengo ya kuanzishwa kwa taasisi zenu,” alisema.
Mafuru alisema taasisi ambazo uzalishaji wake umeshuka lakini gharama za uendeshaji ziko juu, hazina budi kupunguza wafanyakazi ili kulingana na mapato yake.
“Kama hawataweza kufanya hivyo, watafute njia nyingine ya kuongeza uzalishaji kwa kutumia wafanyakazi walionao. Kwenye sekta binafsi, kampuni ikianza kufanya vibaya inapunguza matumizi yake na moja ya njia wanazotumia ni kupunguza wafanyakazi. Huku serikalini utasikia mtendaji mkuu akiandika barua, siyo proposal (mradi), kuomba fedha kwa ajili ya mtaji. Hatuwezi kwenda mbele,” alisema.
Mafuru aliyasema hayo jana katika mkutano maalumu ulioitishwa kwa maagizo ya Rais John Magufuli ili kuwakumbusha watendaji mbalimbali wa taasisi na mashirika ya umma nchini, juu ya wajibu wao katika kuwahudumia wananchi.
Mkutano huo uliwahusisha wenyeviti wa bodi, wajumbe wa bodi na watendaji wa taasisi na mashirika mbalimbali ya umma ambayo kwa sasa yamefika 216, yakiwa na mali zenye thamani ya Sh20 trilioni.
Hata hivyo, alisema pamoja na mtaji huo, taasisi na mashirika ya umma yamekuwa yakichangia Sh185 bilioni kwenye Pato la Taifa.
“Kwa mtaji wa Sh20 trilioni, hicho ni kiasi kidogo sana ambacho kinarudi serikalini. Kwa wenzetu wa sekta binafsi, ukimpatia mtaji huo basi baada ya muda fulani unamkuta kapata mara mbili ya mtaji aliopewa,” alisema Mafuru ambaye amefanya kazi kwenye taasisi za benki kwa miaka 15.
Alisema Rais Magufuli amemtuma kuwakumbusha kila mmoja kwenye taasisi yake ahakikishe anapunguza kero zote zinazopatikana kwa kutumia rasilimali alizonazo.
Alisisitiza kuwa kila mmoja atambue kwamba anawajibika katika kuleta maendeleo ya Taifa hili.
Msajili huyo aliongeza kuwa Serikali imekuwa hainufaiki na mashirika ya umma ambayo ndiyo yangekuwa msaada mkubwa wa kupunguza mikopo ambayo inadaiwa.
Hata hivyo, alisema mashirika yamekuwa yakiiacha kulipa madeni hayo licha ya kwamba yanapata faida kubwa kila mwaka.
“Siyo lazima faida inayopatika kwenye taasisi na mashirika ya umma irudi serikalini, lakini mashirika yenyewe yanaweza kusaidia katika shughuli mbalimbali za maendeleo ambazo Serikali ilitakiwa kufanya” alisema.
Mafuru alitoa mfano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) akisema linapopata faida kubwa, linaweza kuamua kujenga kipande cha reli kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro na kuisaidia TRL na Serikali.
Wabunge kutopewa posho
Mafuru alisema wabunge ambao ni wajumbe wa bodi za mashirika hayo, hawatalipwa posho za vikao vya bodi kwa sababu wanalipwa posho hizo kwenye kamati zao.
Alisema kuendelea kufanya hivyo ni sawa na kuwalipa posho mara mbili kwa kazi moja, jambo ambalo halikubaliki.
Alisema kuna mpango wa kuwaondoa wabunge kwenye bodi hizo ili washiriki kikamilifu kuisimamia Serikali na kwamba mbunge anapokuwa sehemu ya bodi anakosa uhuru wa kufanya kazi yake kama mwakilishi wa wananchi.
“Shirika linapofanya vibaya wajumbe wote wa bodi wanahusika bila kujali ni mbunge au la. Kuna mbunge mmoja alipata msukosuko wakati wa sakata ya Tanesco, kwa hiyo tunajaribu kuwalinda ili wafanye kazi yao kikamilifu,” alisema.
Kuhusu uteuzi wa wenyeviti wa bodi, Mafuru alisema Rais anawateua kwa sababu anaamini wana uwezo wa kusimamia na kuongoza bodi hizo ili kuleta matokeo chanya.
Alisema wenyeviti wengi wamekuwa wakichukulia nafasi wanazopewa kama zawadi na kushindwa kusimamia majukumu ya mashirika au taasisi husika.
Alisisitiza kuwa uenyekiti ni jukumu kubwa ambalo linahitaji kuifahamu taasisi vizuri ili kutoa maamuzi sahihi.
Aliwataka wenyeviti wa mashirika ya umma kutambua wajibu wao na kuondokana na dhana kwamba wanapoteuliwa basi wanapewa ‘ulaji’.
Kwa upande mwingine aliyataka mashirika hayo kufanya ukaguzi wa hesabu zao na kuwasilisha ripoti katika ofisi yake.
Akitoa maoni yake kuhusu uendeshaji wa mashirika ya umma, Mkuu wa Taasisi ya UsiMamizi wa Fedha (IFM), Profesa Emmanuel Mjema, alisema Wakala wa Manunuzi ya Serikali (GPSA) amekuwa tatizo ambalo linapaswa kuangaliwa. Pia, alisema Wakala wa Huduma za Ufundi na Umeme (Temesa), nao wamekuwa ni tatizo kwa kutopeleka magari kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo huku wakitoza fedha, lakini wanaambiwa wapeleke magari hayo GS Motors.
Mafuru alisema amepokea maoni hayo na kuongeza kuwa ofisi yake imekuwa ikipata malalamiko kutoka mashirika mbalimbali kuhusu GPSA na kuahidi kufuatilia na kuyapatia ufumbuzi wa kudumu.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Albina Chuwa alitaka mishahara ya watendaji wa taasisi na mashirika ya umma iangaliwe upya kwa sababu wapo wanaopata mikubwa kiasi cha Sh36 milioni wakati wengine wanapokea Sh3 milioni.
Comments
Post a Comment